Jamii nchini, imeaswa kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kuyaweka mazingira katika hali ya usafi ili kujikinga na Magonjwa ya Mlipuko.
Rai hiyo imetolewa na Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Dkt. Kisaka Deo mara baada kufanya ziara katika visiwa vya Goziba, Kerebe na Nyaburo vilivyo ndani ya ziwa Victoria kwa ajili ya kujionea namna elimu ya afya ilivyozaa matunda katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema, “ili kujikinga na Magonjwa yote lazima tuyaweke mazingira yetu katika hali ya usafi,unaponawa mikono haujikingi na Marburg pekee inasaidia pia kwa kujikinga na magonjwa kama vile kuhara,Kipindupindu, kuumwa tumbo.“
Katika hatua nyingine Dkt. Kisaka amewahimiza akina mama wajawazito kubadili tabia na kuwa na desturi ya kuwahi kliniki mapema pamoja na kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata chanjo mbalimbali.
Nao baadhi ya viongozi katika visiwa hivyo, akiwemo Afisa Mtendaji kata ya Kerebe, Kanali Sefu Muya, diwani kata ya Kerebe Sudy Said Self pamoja na diwani kata ya Goziba Mataba Mataba wamesema Serikali imekuwa ikichukua hatua katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.