Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amewaapisha wabunge 19 wa Viti Maalumu kutokea Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hii leo kwenye Viwanja vya Bunge, Jijini Dodoma.
Wabunge hao walioapishwa ni pamoja na waliowahi kuwa wabunge kupitia chama hicho katika Bunge la 11 ambao ni Halima Mdee (Aliyekuwa Mbunge wa Kawe), Esther Matiko (Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini), Ester Bulaya (Aliyekuwa Mbunge wa Bunda Mjini), Anatropia Theonest, Jesca Kishoa na Grace Tendega.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Viti maalum wa CHADEMA walioapishwa hii leo na Spika, Halima Mdee amesema watawatumikia wananchi kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata maendeleo.
“Nikuhakikishie mheshimiwa spika tutafanya kazi kwa uaminifu kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na kwa uadilifu mkubwa kwa viwango vilevile tulivyokuwa tunavifanya. Kuna vijana wapya sisi kama dada zao tunakuhakikishia watafanya kazi bora. Niwahakikishie wana Chadema tutafanya kazi mliyotutuma kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana,” amesema Halima.
Kwa upande wake Spika wa Bunge Job Ndugai amesema atawapa ushirikiano mkubwa wabunge hao ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao ya kuwatumikia wananchi wakiwa Bungeni.
“Kwanza niwapongeze kwa kula kiapo na kuwa wabunge katika Bunge la 12, lakini pia niwaahidi mimi kama spika nitawapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yenu licha ya uchache wenu,” amesema Spika Ndugai.
Wabunge 19 waliopishwa hii leo Novemba 24, 2020 ni Halima Mdee, Grace Tendega, Ester Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Kaiza, Nuzrat Shaban Hanje, Jesca Kishoa, Stella Simon Fiao, Hawa Mwaifunga, Felista Deogratius Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunt Majala, Tunza Malapo, Asna Mohamed, Anatropia Theones, Salome Makamba, Conjesta Rwamulaza.