Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewakabidhi kiasi cha shilingi milioni 30 (15mil kila mmoja) wabunifu wawili wa umeme mkoani Njombe ili ziweze kuwasaidia katika kuboresha miundombinu yao.
Akizungumza wakati akikabidhi fedha hizo mbele ya wananchi wa kijiji cha Lugenge kilichopo katika halmashauri ya mji wa Njombe mkoani humo, mkurugenzi mtendaji wa Tanesco Dkt. Tito Mwinuka amesema kuwa lengo la kufika katika kijiji hicho ni kutimiza ahadi waliyoitoa mbele ya Rais, huku akiahidi kushirikiana na wabunifu hao ili kuongeza nguvu ya umeme katika vijiji vya wabunifu hao.
“Kama tulivyoahidi tulituma wataalamu wamefika hapa tangu juzi na wameweza kubaini ni vitu gani vikifanyika basi vinaweza kusaidia ule umeme upatikane mwingi zaidi na wananchi waweze kufaidika, kwa hiyo kwa maeneo hayo mawili tumeona kuna uwezekano wa sisi Tanesco kusaidia umeme kupatikana mkubwa zaidi kule Msete na hapa Lugenge, uwe salama zaidi na watu waweze kufaidika,”amesema Dkt. Mwinuka
Kwa upande wake, John Fute mbunifu wa umeme katika kijiji cha Msete unaozalisha kilowati 28, mara baada ya kupokea fedha, ametoa rai kwa wananchi kuendeleza vipaji vya watoto wao.
Naye, Lainery Ngailo mbunifu wa umeme katika kijiji cha Lugenge unaozalisha kilowati 15 ameishukuru serikali kwa kuwafikisha wataalamu katika kijiji chake na kuahidi kushirikiana nao ili kuwafikishia nishati wananchi.
Nao baadhi ya wananchi katika kijiji cha Lugenge wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwaona wataalamu hao kutokana na kuwepo kwa wataalamu wengi vijijini wanaoweza kufanya mambo makubwa lakini wamekuwa wakikosa ushirikiano na baadhi ya taasisi za serikali.