Wafanyabiashara na watumiaji wa soko la sabasaba lililopo jijini Dodoma wapo katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kutokana na mlundikano wa uchafu uliopo ndani ya soko hilo.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na mjumbe wa uongozi wa mpito wa soko hilo, Mabewo Daudi ambapo amesema kuwa mlundikano huo unatokana na jiji kutoondoa uchafu huo kwa wakati na kusababisha kuwepo pia kwa harufu kali.

Amesema kuwa kuwepo kwa uchafu huo kunaweza kuhatarisha mlipuko wa magonjwa ya tumbo kwa wafanyabishara wenyewe na hata kwa watumiaji wa soko ambalo kwa hivi sasa limekuwa likiendesha shughuli nyingi kutokana na kuwepo kwa watu wengi.

“Hali ni mbaya kutokana na uchafu uliopo kwenye eneo hili la dampo ambalo limo ndani ya soko hili, suala ambalo linatufanya tushindwe kufanya shughuli zetu kwa uhuru kama ilivyokuwa kwenye masoko mengineyo,”amesema Daudi

Aidha, kwa upande wake, Mwajuma Hassan mama anayejishughulisha na upikaji wa chakula amesema kuwa ili kuondokana na kero hiyo, jiji wanatakiwa kujaza kifusi ambacho kitaondoa tope linalotokana na mvua zinazoendelea kunyesha

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya mazingira na udhibiti wa taka ngumu jijini Dodoma, Dickson Kimaro amesema kuwa tatizo lililopelekea kuchelewa kuondoshwa kwa taka katika eneo hilo la soko la sabasaba, kuwa linatokana na mvua kubwa zinazozoendelea kunyesha mkoani humo na kusababisha magari ya kusomba taka kushindwa kufika eneo hilo la dampo.

Hata hivyo ameongeza kuwa pamoja na changamoto hiyo bado juhudi kubwa zinaendelea kufanywa na kampuni ya Green waste Ltd ambayo yenye dhamana ya kuondoa taka katika jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Halmashauri na idara ya Mazingira kuhakikisha taka hizo zinaondolewa haraka.

 

CCM Njombe wapiga marufuku michango, viongozi washushwa vyeo
Wabunge wa CCM wampongeza CAG