Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua kituo cha Tiba Mtandao cha Taifa kilichopo Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) ambacho kitawahudumia wagonjwa wa hospitali za halmashauri, wilaya, rufaa na hospitali nyingine nchini.
Kabla ya kuzindua kituo hicho, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameagiza mradi wa tiba mtandao kuunganishwa katika hospitali ya vituo vya afya, hospitali za halmashauri, Wilaya na hospitali za rufaa ili kuwafikia wananchi wengi ambao hawana uwezo wa kwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), MOI, Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwete (JKCI) pamoja na hospitali nyingine zinazotoa huduma za ubingwa wa juu.
“Naagiza muanze kuanganisha tiba mtandao na hospitali za rufaa za mkoa 28, halmashauri zaidi ya 145. Lakini wataalamu wetu wa mawasiliano jaribuni kuunganisha nchi za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Comoro,” amesema Waziri Ummy.
Amebainisha kwamba picha za X-ray na ultrasound pamoja na picha nyingine kutoka hospitali za halmashauri, wilaya, hospitali za rufaa nchini zitatumwa kwenye kituo cha tiba mtandao na kusomwa na madaktari bingwa na majibu kurejeshwa kwenye hospitali hizo.
“Wataalamu wetu wabobezi watatumia tiba mtandao kuwahudumia maskini ambao wanahitaji huduma za kibingwa,” amesema Waziri wa Afya.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Abel Makubi akizungumza kutoka Mkoa wa Morogoro kwa njia ya mtandao, amesema tiba mtandao ni kielelezo kwamba huduma za afya zimeboreshwa ili wananchi wengi waweze kufikiwa na wataalamu wa afya.
Amesema tiba itapunguza rufaa kutoka katika hospitali za mikoa pamoja na kupunguza gharama kwa wagonjwa mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Tiba katika Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe amesema tiba mtandao itapunguza kero ya wagonjwa kusafiri kwenda kutafuta tiba katika hospitali zinazotoa huduma za kibingwa nchini.
Dkt. Magembe amesema pia tiba mtandao itatoa fursa kwa madaktari bingwa kuwajengea uwezo watalaamu wa afya kwenye hospitali za halmashauri, wilaya na hospitali za rufaa nchini.