Wahudumu wa Afya wametakiwa kuhakikisha wanalinda usalama na ubora wa Mgonjwa wanapotenda majukumu yao ili kuwafanya wagonjwa wawe na amani wanapofika katika vituo vya huduma za afya.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Tanzania Matilda Ngalina wakati wa maadhimisho ya Siku ya usalama wa wagonjwa Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Agakhan jijini Dar es salaam.

Dkt. Ngalina amesema wagonjwa wana haki kubwa ya kulindiwa usalama wao pindi wanapofika kupata huduma za afya, na wengi wanaamua sehemu ya kutibiwa kutokana na aina ya huduma wanayoipata.

Dkt. Ngalina ameongeza kuwa mhudumu wa afya anatakiwa kuhakikisha kila mgonjwa anaepita katika mikono yake haondoki na malalamiko yoyote kwa sababu inapunguza uaminifu kwa hospitali husika na pia ngonjwa anakosewa haki yake.

Nae Nyangelu Goya ambae ni Mratibu wa Kitengo cha usalama na ubora wa Mgonjwa kutoka hospitali ya Agakhan amesema kila hospitali inatakiwa kuandika kuweka kitengo hicho kwa kuwa kinasaidia kulinda haki za wagonjwa na sifa za hospitali hivyo kupunguza vifo na madhara yanayotokana na huduma hafifu.

Siku ya Usalama wa Mgonjwa Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 17 Septemba ambapo mwaka huu kauli mbiu ya shirika la afya duniani ni “Uzazi salama na Utunzaji wa Watoto wachanga” ambapo WHO imewataka wahudumu wa afya kuanza sasa kusimamia usalama wa mjamzito na kuheshimu uzazi.

Takwimu za shirika la afya Duniani zinasema Inakadiriwa kuwa zaidi ya wajawazito 800 hufariki kila siku duniani kutokana na sababu tofauti za matatizo ya uzazi na zaidi ya watoto wachanga 6000 hufariki kila siku kutokana na huduma mbovu na kutojali usalama wa mgonjwa.

Orodha ya wachezaji wanaokwenda Nigeria
Muongozo wa mpango wa kuwapanga wamachinga