Takwimu za vifo vitokanavyo na uzazi katika Kanda ya Magharibi mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2019 inaonesha akina mama wajawazito 210 walipoteza maisha ambapo Kigoma vifo 100, Tabora 62 na Katavi 48.
Hayo, yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian katika ufunguzi wa kikao cha watalaam wa Afya Kanda ya Magharibi, inayounda mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma cha kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika kanda hiyo.
Amesema, mwaka 2020 akina mama 235 walipoteza Maisha ambapo Kigoma vilikuwa vifo 119, Tabora 58 na Katavi 58, na mwaka 2021 akina mama 174 wakipoteza maisha ambapo Kigoma vilikuwa vifo 75, Tabora vifo 58 na Katavi vifo 41.
Aidha, amezitaja sababu za vifo vya wajawazito kuwa ni pamoja na tutokwa damu nyingi baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, kupasuka mfuko wa Uzazi, kutokwa na damu nyingi kabla ya kujifungua, upungufu mkubwa wa damu, uambukizo wakati na baada ya kujifungua.
Kuhusu hali ya vifo vilivyotokana na uzazi kitaifa kwa mwaka 2020, Mkuu huyo wa Mkoa amesema vilikuwa ni 1,640 na mwaka 2021 vilikuwa 1,588 na kwamba takwimu za vifo vya watoto wachanga kuanzia siku 0-28 katika Kanda ya Magharibi kwa mwaka 2021 ni watoto wachanga 2,539.
Vifo hivyo vya watoto kwa kwa upande wa Kigoma vilikuwa ni 1,026, Tabora 954, na Katavi 559 vikisababishwa na kushindwa kupumua, watoto kuzaliwa njiti, uambukizi kwa watoto wachanga na kuzaliwa na uzito pungufu.