Eva Godwin, Dodoma.
Mtandao wa Jinsia Tanzania – TGNP, umetoa mafunzo kwa Wanahabari kuhusu Uandishi wenye kuzingatia mrengo wa kijinsia hususani katika kuhamasisha mila na Mitazamo chanya yenye kuongeza ushiriki wa Wanawake katika Uongozi.
Akizungumza katika mafunzo hayo yanayoendeleoa jijini Dodoma, Mwezeshaji Ananilea Nkya amesema Wanahabari wana uwezo wa kuandika habari muhimu za kuwezesha idadi kubwa ya Wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi.
Amesema, “Wanahabari mnauwezo mkubwa wa kuhamasisha Wanawake kushiriki nafasi za mbalimbali za Uongozi, tunawatumia ninyi kwasababu mnasauti na pia mnajua kuhamasisha suala hili, Mwanamke hapaswi kuwa nyuma, kila mmoja ana haki ya kushiriki chochote kwenye Jamii.”
Nkya ameongeza kuwa, Mwanamke akipata nafasi ya Uongozi kwenye jamii anao uwezo wa kuongoza vyema kuliko Mwanaume, kwani huwa na uoga wa kutojihusisha na mambo yanayoweza kuwasababishia au kuwaingiza kwenye matatizo.
Aidha ameongeza kuwa, “kuna kauli ambazo zinawakatisha tamaa Wanawake na kushindwa kushiriki katika suala la uongozi kwenye Jamii, kuna msemo kama Mwanamke ni kiumbe dhaifu, hana maamuzi na misemo mingine mingi.”
Mtandao wa Jinsia Tanzania – TGNP, unatambulika kwa harakati zake za wanawake na asasi za kiraia nchini, Afrika na kwingineko kwa kujihusiasha na ukuzaji wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji kwa wanawake nchini.