Jeshi la Kujenga Taifa, JKT limesema vijana 147 waliokutwa na maambukizi ya VVU si wale ambao tayari wapo ndani ya mafunzo ya jeshi hilo kama wengi wanavyodhani na limekemea baadhi ya vyombo vya Habari kutumia picha za vijana ambao si wahusika na kuzua taharuki kwa jamii.
Taarifa hiyo, imetolewa jijini Dodoma na Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena kufuatia kutolewa kwa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kwa kipindi cha Februari 2022 hadi Februari 2022 iliyowasilishwa wiki iliyopita.
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema wale waliokutwa na maambukizi ya VVU walipatiwa huduma za kiafya ikiwa ni pamoja na kupewa ushauri nasaha, na wengine wakaanzishiwa dawa za kufubaza ugonjwa huo.
Wiki iliyopita, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi ililitaarifu Bunge kuwa vijana 147 kati ya 67,299 waliojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa mujibu wa sheria, katika kipindi cha miaka mitatu (2019-2021), wamekutwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), sawa na asilimia 0.22 kwa vijana waliomaliza kidato cha sita nchini, na kuitwa kujiunga na JKT.