Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza amekabidhiwa Tuzo yake ya Mchezaji Bora wa Mashabiki wa Simba SC mwezi Januari (Emirate Aluminium Profile Simba Fans Player of the Month).

Baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo, Ntibazonkiza amewashukuru wachezaji wenzake kwa ushirikiano waliompa uwanjani, benchi la ufundi kumpa nafasi na mashabiki waliompigia kura kwa wingi.

Saido amesema amesajiliwa kwa ajili ya kuisaidia timu kufanya vizuri na amefurahi kuona msaada wake uwanjani pamoja na wenzake unafanya vizuri.

“Nimefurahi kupata tuzo hii, ina maana kubwa kwangu. Nawashukuru familia yangu, wachezaji, benchi la ufundi pamoja na mashabiki kwa ushirikiano huu mkubwa.”

“Pia nawashukuru wadhamini Emirate Aluminium Profile kwa kutuandalia tuzo hii, bahati nzuri naifahamu Emirate maana hata kwetu Burundi ipo. Inatuongezea morali wa kuipambania timu siku zote,” amesema Saido.

Katika mwezi Januari, Saido amecheza michezo mitatu sawa na dakika 270 akifunga mabao mawili na kusaidia kupatikana kwa lingine moja.

Saido amekabidhiwa pesa taslimu Shilingi Milioni Mbili (2,000,000) na Tuzo kutoka kwa wadhamini Emirate Aluminium Profile kama sehemu ya zawadi ya kuibuka mshindi.

Wawili wakamatwa na Lori la Spirit, boksi za Pombe bandia
Waliokutwa na VVU JKT wapewa huduma maalum