Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, kuhakikisha wafanyabiashara wote waliopanga meza katikati ya barabara za mitaa, Kariakoo na Msimbazi kuondolewa ili barabara zibaki wazi kwa ajili ya magari kushusha mizigo.

Ametoa maagizo hayo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya kuwapanga machinga kwa kila Wilaya huku akisisitiza katika siku zilizobaki kufikia Oktoba 18, 2021 serikali itaongeza nguvu kwenye kutoa matangazo na elimu na kuhakikisha kila mfanyabiasahara anakuwa katika eneo alilopangiwa.

Aidha RC Makalla pia ameelekeza maeneo yote watakayopelekwa wafanyabiashara ikiwemo masoko, daladala zishushe abiria kwenye maeneo hayo ili kuchochea biashara.

Sambamba na hayo yote RC Makalla maewasihi wafanyabiashara wote wanaofanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa kutumia vizuri siku zilizobaki kuhama ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Miongoni mwa wafanyabiashara wanaotakiwa kupangwa ni wale waliojenga vibanda juu ya mitaro na mifereji, wanaofanya biashara kwenye maeneo ya watembea kwa miguu, wanaofanya biashara kwenye hifadhi ya barabara, wanaofanya biashara mbele ya maduka, na wanaofanya biashara kwenye taasisi za umma zikiwemo shule.

Miss Kiziwi Tanzania na Elimu ya Afya ya uzazi
DJ Venture awapa somo Wadau wa Muziki Tanzania