Wapiginaji wenye silaha wamewaua takriban watu 19 wakiwemo wanajeshi 10 baada ya kushambulia vijiji viwili Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Jumamosi, muda mfupi baada ya Rais Felix Tshisekedi kutangaza kwamba Mikoa miwili Mashariki mwa nchi hiyo Ituri na Kivu Kaskazini imezingirwa .
Ongezeko la mashambulizi ya makundi yaliyojihami na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa umoja wa mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo.
Shambulio la hivi punde limefanyika siku ya Jumamosi wakati wapiganaji wenye silaha waliposhambulia vijiji viwili katika mji wa Kivu kaskazini wa Beni, mamlaka za jimbo hilo zimesema.
Baadaye siku hiyo Imam mwenye ushawishi mkubwa aliuawa kwa kupigwa risasi msikitini mjini Beni alipokuwa akiwaswalisha watu wakati wa jioni.
Alitambulika kwa kupinga itikadi kali za kidini kupitia kituo kimoja cha redio katika jimbo hilo.