Serikali nchini, imedhamiria kuimarisha huduma za afya huku uwepo wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote ukitajwa kusaidia kuboreshwa kwa huduma bora zitakazomuwezesha kila mwananchi kupata matibabu popote nchini.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya, Edward Mbaga ameyasema hayo katika semina kwa wahariri na waandishi wa habari juu ya sheria ya Bima ya Afya kwa wote iliyofanyika Oktoba 12,2022 Jijini Dar es Salaam.

“Katika kutekeleza mpango huo Serikali itahakikisha kunakuwepo na mazingira wezeshi ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba sambamba na uwepo wa wataalamu wa kutosha katika vituo vya afya na hospitali zote kubwa nchini,” amesema Mbaga.

Ameongeza kuwa, “Bima itampa uhakika mwanachi kupata matibabu kwa haraka kwa kiwango kilekile alichochangia wakati wote pale anapokwenda katika kituo cha Afya au hospitali kubwa.”

Awali, akiwasilisha mada kwa washiriki wa semina hiyo juu ya mapendekezo mbalimbali yaliyopo katika rasimu ya Sheria hiyo, Mjumbe wa Sekretarieti ya Mchakato wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote, Janethi Kibambo amesema kupitishwa kwa sheria hiyo kutaleta manufaa kwa jamii.

Kwa upande wake, Kamishna wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware alisema mamlaka hiyo imejipanga vyema kuhakikisha inasimamia na kuhakiksha huduma bora za bima ya afya zinatolewa kwa wananchi wote.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 14, 2022     
Kisa Ebola: Museveni apiga marufuku 'Sangoma'