Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana leo tarehe 12 Oktoba, 2022 amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA aliyoiteua hivi Karibuni, ambapo amesema uteuzi wa bodi hiyo umefanyika kwa umakini, kuzingatia weledi na uzoefu wa wakurugenzi hao utakaosaidia utekelezaji wa mikakati ya kuzuia ujangili, kuongeza idadi ya watalii na mapato na hivyo kuendeleza sekta ya Wanyamapori.

Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi iliyofanyika Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro, Dkt. Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kwa kumteua Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA na kuwapongeza wajumbe Wote wa Bodi hiyo kuteuliwa kuiongoza TAWA.

Amesema, “Nichukue nafasi hii Kumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kumteua “Chairman” (Mwenyekiti) wetu Mej. Jen.(Mstaafu) Hamis Semfuko asante sana ametuletea “Chairman” hodari kabisa na Kwakweli tuna matumaini makubwa sana na wewe kwa dhati kabisa nawapongeza Wakurugenzi wa Bodi wote Kwa kuteuliwa kuiongoza Bodi hii ya TAWA.”

Aidha, amesema ametoa rai Kwa bodi hiyo Kuweka mikakati ya Changamoto ya ongezeko la matukio ya Wanyamapori wakali na Waharibifu na uvamizi wa mifugo hifadhini, na kuwataka watu wenye tabia ya kuingiza mifugo ndani ya hifadhi kuacha vitendo hivyo mara moja.

Dkt. Chana ameongeza vitendo vya kuingiza mifugo hifadhini vinaleta athari kubwa Kwa kukausha vyanzo vya maji, kuharibu mazingira na athari zake kuwa kubwa Kwa Taifa, hivyo amewaomba wananchi washirikiane na Serikali katika kuhifadhi maeneo huku akizindua mitambo mbalimbali iliyonunuliwa na TAWA Kwa fedha za UVIKO – 19, ikiwemo mashine za kuchima visima vya maji, matreka, “caterpillars”, boti na maalumu kwa ajili ya doria.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Elaimani Sedoyeka amesema TAWA ina takribani asilimia 10 ya maeneo yote Nchini, hivyo anatumaini kwamba itabuni mikakati mbalimbali ya kuongeza idadi ya watalii, mapato na kuimarisha shughuli za Uhifadhi, kuboresha miundombinu ya Utalii, kujenga uwezo wa watumishi pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi na tija kiutendaji.

Akielezea mikakati ya Bodi mpya ya TAWA, Mwenyekiti wa Bodi Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema mkakati wa kwanza ambao Bodi itaupa kipaumbele ni kupunguza migongano kati ya watu na Wanyamapori “Human Wildlife Conflicts” Ili kuhakikisha TAWA inakuwa chombo ambacho kinakuwa na faida Kwa Serikali na Umma.

Kamishna wa Uhifadhi TAWA ambaye pia ni Katibu wa Bodi iliyozinduliwa leo, Mabula Misungwi Nyanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Kwa kumteua Mej. Jen. Mstaafu Hamis Semfuko kwa awamu nyingine Ili aendelee kufanikisha kazi kubwa aliyokwisha ianzisha.

Rais Samia azindua chuo cha VETA Kagera
Majaliwa atoa neno kwa NSSF maonesho ya Vijana Kitaifa