Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amewataka wananchi wa Taifa hilo kuendelea kuvumilia adha ya makali ya maisha inayowakabili, wakati Serikali ikijaribu kufufua uchumi na kutafuta suluhu ya tatizo hilo.
Akizungumza huku akionekana kuutetea muswada mpya wa Fedha 2023 unaotarajia kupitishwa na Bunge, Gachagua alisema ni sahihi kwa serikali kufanya maamuzi magumu na yasiyopendeza kwa manufaa ya watu wake.
Amesema, “pindi tu Bunge la Kitaifa litakapopitisha Mswada huo, utasaidia serikali kupata pesa kufufua uchumi lakini kwa sasa tuna deni la Sh9.6 trilioni kwa hivyo ni lazima tukusanye ushuru wa kujenga barabara na kuendeleza miradi mingine.”
Gachagua ambaye alikuwa akizungumbe mbele ya madhabahu ya Kanisa la Kianglikana la Nyahururu Kaunti ya Laikipia, ameongeza kuwa “ili mambo yabadilike lazima watu waumie kidogo. Hii ndiyo maana tunaomba Wakenya watupe muda ili tusuluhishe masuala ya kupanda kwa gharama ya maisha.”