Idadiya watu wanaofariki kwa kunywa sumu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro imetajwa kuongezeka huku rika la vijana ambao ndio nguvukazi ya taifa likiongoza.
Wakizungumza na gazeti la Mtanzania wakazi wa wilaya hiyo wameelezea kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya watu kunywa sumu na kukatisha maisha yao, wakidai kuwa matukio ya watu kunywa sumu yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Juma Hussein mkazi wa Sanya juu akizungumza na gazeti hilo ameeleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikileta hofu na simanzi miongoni mwa jamii.
“Haipiti wiki utasikia fulani kafa kwa kunywa sumu au kalazwa, tunaomba viongozi wa dini watusaidie kekemea tabia hiyo na wafanye maombi au dua maalum katika nyumba za ibada ili kuiponya jamii. Nawashauri wale wenye changamoto za kimaisha wasikatishe uhai wao bali waeleze wazi tatizo ili wapewe ushauri,”amesema Hussein.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Siha, Peter Msaka ametaja baadhi ya sababu zinazoelezwa kuchangia vijana kunywa sumu kuwa ni ugomvi wa kifamilia, wivu wa kimapenzi na msongo wa mawazo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Siha, Dkt. Nsubili Mwakapeje amesema kuwa vifo vitokanavyo na sumu vinaweza kuepukika na kwamba wanaangalia uwezekano wa kuweka sheria katika kupambana na hilo.
‘Tunaangalia uwezekano wa kuweka sheria ili watu wanaokunywa sumu na kupona wachukuliwe hatua, hii sheria itatoa angalizo kwa jamii kuwa tabia hiyo sio nzuri na haikubaliki na yewyote anayefanya kitendo hicho atachukuliwa hatua,”amesema Dkt. Mwaipeje.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwakapeje, kuanzia mwezi Januari hadi Novemba 12 mwaka huu, jumla ya waliokunywa sumu za aina mbalimbali ikiwamo Gramoxone walikuwa 59 ambapo wanaume walikuwa 29 na wanawake 30 na kati ya hao 17 walifariki Dunia.