Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Daniel Chongolo amewaonya wananchi wa jimbo la Isimani mkoa wa Iringa kuacha kuuza ardhi kiholela badala yake waitumie kuleta tija na kukuza uchumi wao.
Chongolo ametoa kauli hiyo Kutokana na idadi kubwa ya watu wanaohitaji mashamba kuhamia katika eneo la Pawaga, Jimbo la Isimani inakojengwa skimu ya Umwagiliaji inayogharimu Sh55 Bilioni, ambapo kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi kuuza ardhi bila sababu za msingi.
Amesema “acheni kuuza ardhi hovyo ardhi ndio dhahabu ya uhakika kama unataka fedha mwambie mtu mwaka huu sitaki kushika jembe,lima ardhi yangu hii nipe fedha mwakani nirudishie ardhi yangu ndio mtu mjanja anavyofanya, acheni kuuza ardhi hovyo mtakuja kujuta na mtakuja kulaaniwa na watoto na wajukuu zenu.”
Amesema mwenye akili haachii ardhi yake kwa ajili ya kumuuzia mtu mwingine anamkodisha ili iendelee kuwa sehemu ya msaada kwake yeye kwa watoto na wajukuu na kuongeza kuwa watu wanapoenda kufuata ardhi vijijini kwani hawajui kama inatija? Hawajui inafaida? Hawajui maslahi yake kwani ninyi hamtaki hiyo tija kwanini mnakaa kienyeji
Chongolo yupo Iringa kwa ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani, kuhamasisha uhai wa Chama ngazi za mashina pamoja na kusikiliza na kukatua kero za wananchi, akiwa ameatana na. Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Sofia Mjema na Katibu wa NEC, Oganaizesheni, Issa Haji Gavu.