Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema hadi kufikia Aprili mwaka huu serikali ilikuwa imetoa shilingi 30.9 bilioni kwa vikundi 5,120 vya wanawake kwa Halmashauri 184 Nchini kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake na wanaume kuboresha kipato na kuondoa umaskini.
Akisoma hotuba ya Makamu wa Rais jijini Dodoma Leo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima katika hafla ya uzinduzi wa program ya ANAWEZA iliyofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Kifedha la Benki ya Dunia (IFC), amesema fedha hizo zimetolewa kupitia sheria ya fedha za mamlaka za serikali za mitaa.
Awali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe amesema kuwa Rais wa Zanzibar Dk. Husein Ally Mwinyi anathamini kazi zinazofanywa na wanawake ambapo amekuwa akiwateu kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema, “tunathamini kazi nzuri zinazofanywa na Wanawake, na ukiona Mwanaume anamafanikio ujue nyuma yake kuna Mwanamke mchapakazi, mwenye akili na kujitambua.”
Awali Mkurugenzi Kanda wa IFC Jumoke Jagun-Dokunmu, alisema program ya ANAWEZA itatekelezwa kwa miaka mitano na inalenga kushughulikia changamoto zilizopo ili kuwezesha ushiriki wa wanawake katika sekta binafsi.
“Nafasi za uongozi na ujasiriamali wenye ufanisi endelevu na programu hiyo itagharimu fedha za Kimarekani milioni 7.5, inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano,” amesema.