Polisi nchini Iran imeanzisha msako wa kuwakamata Wanawake wasiofunika nywele zao katika maeneo ya hadhara wakidai kitendo hicho kinakiuka kanuni za mavazi za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Iran, Saeed Montazer Almehdi imeeleza kuwa Polisi watatumia magari na miguu katika msako huo, ili kutoa tahadhari, kuchukua hatua za kisheria na kuwapeleka Mahakamani wote wasiotii amri na kupuuzia zoezi hilo.
Hata hivyo, chama cha kihafidhina chenye idadi kubwa ya wabunge na nafasi kubwa katika uongozi kimekuwa kikitetea kanuni za mavazi, kutokana na Wairani wengi kutaka mabadiliko.
Mwezi Mei 2023, Mahakama na Serikali zilipendekeza muswada wa kuunga mkono utamaduni wa hijab na usafi, uliochochea mjadala mzito ndani ya taifa hilo huku hatua hii ikijiri ikiwa ni miezi kumi tangu kilipotokea kifo cha Mahsa Amini, (22), aliyefariki mikononi mwa Polisi kwa kosa kukiuka kanuni za mavazi.