Ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa amewataka wanawake wenye ndoto za kugombea na kushika nafasi mbali mbali za uongozi kuanza harakati za kujijenga mapema ili waweze kuibuka kidedea na kuwa washindi.

Dkt. Mzuri ameyasema hayo wakati alipokua akizungumza na wanawake wawakilishi toka vyama mbali mbali vya siasa visiwani Zanzibar, walioanza mafunzo ya siku tatu ambayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kugombea na kushika nafasi mbali mbali za uongozi zikiwemo za ndani ya vyama vya siasa na hata zile za viongozi wa kuchaguliwa majimboni.

Amesema, kwa muda mrefu wanawake wengi wamekua wakishindwa kutimiza malengo yao licha ya kuwa na nia ya kuwa viongozi na tafiti mbali mbali zimeonyesha kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea ni kutojiandaa mapema.

Baadhi ya wawakilishi katika mafunzo hayo walipokua wakiendelea na mafunzo.

‘’Lazima tutambue kuwa tunakabiliana na changamoto nyingi sana ikiwemo wenzetu wanaume wana hila za kutuhujumu hivyo na sisi wanawake tunapaswa kujiandaa mapema sana na niwaambie tu hakuna kurudi nyuma muda ni sasa,’’aliongezea.

Mkurugenzi huyo pia amewataka washiriki hao wa mafunzo pamoja na wanawake wengine kutokata tamaa licha ya changamoto mbali mbali watakazozipitia zikiwemo za kukatishwa tamaa kwa makusudi na watu wenye dhamira mbaya dhidi yao.

Akizungumzia kuhusu suala la rushwa kwenye uwanja wa siasa, Dkt. Mzuri ameitaka Serikali kupitia mamlaka husika kuhakikisha wanafuatilia kwa umakini zaidi ili waweze kuwabaini na kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanaojihusha na vitendo hivyo na kusisistiza kuwa rushwa ni dhambi na haipaswi kuachiwa ikaendelea kukandamiza haki.

Tanzania yakabidhi rasmi msaada nchini Malawi
Waziri Mkuu ataka mikakati kukitangaza Kiswahili Kimataifa