Wabunge wa Lebanon, kwa mara ya sita wameshindwa kumchagua mrithi wa rais wa zamani, Michel Aoun, ambaye muda wake ulimalizika mwezi uliopita Oktoba, 2022, kutokana na mgawanyiko baina ya wafuasi wa vuguvugu lenye nguvu la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran na wapinzani wake.
Mbunge, Michel Moawad ambaye anaonekana kuwa na ukaribu na Marekani, amepata uungwaji mkono wa kura 43 katika bunge lenye viti 128 lakini hesabu zake zilizidiwa na kura 45 zilizopigwa na wabunge wanaoiunga mkono Hezbollah na hivyo kukosa idadi inayohitajika kwa ushindi.
Mara zote sita, Bunge linapokutana kupiga kura, wabunge wanaoliunga mkono kundi la Hezbollah wamekuwa wakitoka nje kabla ya duru ya pili ya kura.
Kura hiyo, imefanyika wakati Lebanon ikigubikwa na mzozo wa kiuchumi ambao unatajwa na Benki ya Dunia kuwa mbaya kabisa katika historia ya hivi karibuni.