Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya watoto na wasichana, Plan International limesema unyanyasaji wa mitandaoni umesababisha wasichana kuacha kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii.
Utafiti huo mpya uliofanywa na shirika hilo na kuchapishwa siku ya Jumapili uliwajumuisha wasichana na wanawake 14,000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25 kwenye nchi 22 Kwa mujibu wa shirika hilo, takriban wasichana asilimia 60 wamekumbana na unyanyasaji wa mitandaoni.
Mtendaji Mkuu wa Plan International, Anne-Birgitte Albrectsen amesema kuwa wasichana wananyamazishwa kwa kunyanyaswa vibaya mitandaoni. Asilimia 39 ya wasichana walikumbana na unyanyasaji kwenye mtandao wa Facebook, asilimia 23 Instagram, asilimia 14 Whatsapp, asilimia 10 Snapchat, asilimia 9 Twitter na asilimia 6 Tiktok.
Utafiti huo umegundua kuwa mmoja kati ya wasichana watano alikuwa amepunguza au ameacha kutumia kabisa mitandao ya kijamii kutokana na mashambulizi ya aina hiyo. Plan International imesema kuwa mmoja kati ya wasichana 10 alibadili njia anayoitumia kujielezea mitandaoni.
Kulingana na utafiti huo, takriban asilimia 22 ya wasichana waliohojiwa wamesema wao wenyewe au rafiki zao wamebaki na woga kuhusu usalama wao, kwani nusu ya hao wanahofia kunyanyaswa kingono au kimwili.