Na Allawi Kaboyo – Bukoba.

Wakati vyama vya siasa nchini vikiendelea na zoezi la kuomba kuchaguliwa na wananchi kushika nafasi mbalimbali za uongozi, tume ya uchaguzi (NEC) imevitahadharisha vyama hivyo kutovunja sheria za nchi kwa kigezo cha uchaguzi.

Katika hotuba ya mwenyekiti  wa NEC iliyosomwa na mkurugenzi wa mipango, ufatiliaji na tathmini wa NEC  Adam Mkina, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Kagera uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa RAS Kagera leo Oktoba 05, ameeleza kuwa pamoja na masuala yote ya uchaguzi suala la utulivu na amani vinatakiwa kupewa kipaumbele.

Amesema kuwa tume imekuwa ikisisitiza umuhimu wa vyama vya siasa na wagombea kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kampeini zao na kuhakikisha wanaepuka kufanya kampeni ambazo zinaashiria ubaguzi katika  misingi ya jinsia, ulemavu, ukabila, udini, maumbile au rangi.

“Tunaendelea kuwasisitiza vyama na wagombea kuwa kunapokuwa na malalamiko yoyote ya kimaadili basi hatua stahiki zichukuliwe ikiwemo,kuwasilisha malalamiko kwenye kamati za maadili ndani ya muda uliyowekwa na sio kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii,” amesisitiza Adam.

Mkina ameongeza kuwa tume inaendelea kuratibu  kusimamia na kuendesha uchaguzi huu kwa kutumia sheria za uchaguzi, na kuwakumbusha wanasiasa na wananchi kujihadhari na vitendo ama matamshi yanayoweza kusababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi.

Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura umewezesha daftari hilo kuwa na jumla ya wapiga kura 29,188,347 nchi  nzima, ambapo pia wagombea kutoka vyama vya siasa 15 waliteuliwa kugombea nafasi ya urais .

Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi manispaa ya Bukoba ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo amewahakikishia wananchi wa manispaa hiyo kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki hivyo wanao wajibu wa kujiokeza kupiga kura kwaajili ya viongozi wanaowataka.

Mkutano huo umewakutanisha wadau ambao ni waandishi wa habari, viongozi wa dini, asasi za kiraia, watu wenye ulemavu na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na elimu ya mpiga kura.

Chanzo cha ajali iliyoua watano Dar
Wasichana kunyanyasika mtandaoni