Waziri wa zamani wa Kilimo na Chakula, Stephen Wassira amemvaa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu baada ya mbunge huyo kudai kuwa aliwahi kukwepa makonde kadhaa kutoka kwake katika eneo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lissu alidai kuwa Wassira aliwahi kumbananisha katika eneo fulani baada ya kikao cha Bunge kutokana na kuchukizwa na maneno makali aliyoyatoa bungeni dhidi yake, na kwamba alimrushia ngumi mbili ambazo zote alifanikiwa kuzikwepa.

Akijibu madai hayo ya Lissu, Wassira amedai kuwa mwanasheria huyo msomi ni muongo na kwamba hakuwahi kufanya kitendo hicho, na kuongeza kuwa hana heshima hata kwa viongozi wakuu wa nchi.

“Huyu mtu amethubutu kuwatukana marais waliopita, kamtukana Benjamini Mkapa, kamtukana Jakaya Kikwete ambaye alimkaribisha Ikulu na kunywa juisi huku amejikunyata, sasa anamtukana Rais Magufuli,” Wassira anakaririwa na Mwananchi.

“Mimi sio msemaji wa Magufuli , lakini amekuwa anamtukana,” aliongeza mbunge huyo wa zamani wa Bunda Mjini huku akisisitiza kuwa kigogo huyo wa Chadema hana maadili.

Wawili hao wamewahi kusigana pia mahakamani, katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa Bunda Mjini uliompa ushindi Esther Bulaya (Chadema) dhidi yake, ambapo Lissu alisimama kama mwanasheria wa Bulaya.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na wapiga kura wanaomuunga mkono Wassira ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, hivyo kuhalalisha ubunge wa Bulaya.

Chadema wapata pigo, kada atimkia CCM
Magazeti ya Tanzania leo Aprili 3, 2017