Mganga Mkuu Mkoa wa Pwani, Dkt.Gunini Kamba amesema mradi wa Afya Tek umesaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga, huku Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya, Erick Msunyaro akisema mradi huo umesaidia kupunguza gharama ya utumiaji wa karatasi.
Hayo yamebainishwa na Viongozi hao, katika hafla ya majumuisho mara baada ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha, ulitoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo takribani 500 ,vitendea kazi ikiwemo simu za mkononi 450 zenye mfumo wa Afya Tek.
Mradi wa Afya-Tek unatekelezwa katika Halmashauri ya Kibaha na Manispaa ya Kibaha ukiwa na lengo la kuchangia kupunguza vifo vya wajawazito,mama waliojifungua, na watoto chini ya miaka mitano na kuboresha afya za vijana balehe ambapo unatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, TAMISEMI, Baraza la Famasi, Timu za Afya za Mkoa na Halmashauri na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Mradi huo, hutumia mfumo wa teknolojia ya kidijitali kuwaunganisha watoa huduma za afya katika ngazi ya jamii(WAJA),wahudumu wa maduka ya dawa muhimu(DLDM) na vituo vya huduma za afya na umeanza kutumika kuanzia Julai 2020 na hadi sasa umeunganisha watoa huduma ngazi ya Jamii 240,DLDM 149, vituo vya kutolea huduma za afya vya umma 39 na binafsi 10.