Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri wa kufanya uamuzi wa haraka wa kuwarejesha nchini, Watanzania waliokuwa wanaishi Jamhuri ya Sudan.
Dkt. Tax aliwambia waandishi wa habari waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hii leo Aprili 27, 2023 kuwa zoezi hilo la kuwarejesha nyumbani Watanzania hao, lilikuwa na changamoto nyingi lakini hatimaye limefanikiwa na watu hao wamewasili nchini wakiwa salama isipokuwa, wawili ambao wamekumbwa na changamoto za kiafya kutokana na mshituko uliosababishwa na mapigano yanayoendelea nchini humo.
Amesema, safari ya kurejea nchini ya Watanzania hao, ilianza tarehe 24 Aprili 2023 kutoka Jiji la Khartoum hadi mpaka wa kimataifa wa Metema uliopo kati ya Sudan na Ethiopia, wenye umbali wa kilomita 900.
“Baada ya hapo, tarehe 26 Aprili 2023, Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia uliratibu usafiri kutoka mpaka wa Metema hadi mji wa Gondar takriban kilomita 190,” amesema Dkt. Tax.
Aidha ameongeza kuwa, “Kutoka Gondar, ujumbe huo ulisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kuelekea Addis Ababa. Ndege mbili zilitumika ambapo ya kwanza ilisafirisha watu 135 na ndege ya pili ilisafirisha watu 95. Kutoka Jijini Addis Ababa, wananchi hao walisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) hadi Jijini Dar es Salaam.”
Hata hivyo, Dkt. Tax amewashukuru wadau wote walioshiriki zoezi hilo ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais, Balozi za Tanzania, Khartoum na Addis Ababa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kufanya kazi usiku na mchana kufanikisha safari hiyo.
Kwa upande wao, wazazi walioshiriki kuwapokea vijana wao wakiwakilishwa na Bw. Rashidi kilindo, walitoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia zoezi hilo kikamilifu. Walisema Rais Samia amewarejeshea tabasamu lao ambalo kwa wiki kadhaa hawakuwa nalo kutokana na sintofahamu ya watoto wao.