Msemaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka ( DART) maarufu Mwendokasi, Deus Bugaywa amesema kuwa foleni iliyokuwepo leo Agosti 14, katika kituo cha mabasi hayo kilichopo Mbezi Mwisho inatokana na kuwepo kwa foleni kubwa ya magari barabarani hali iliyosababisha mabasi hayo kuchelewa kufika kituoni.
Bugaywa amesema kuwa foleni ya Mbezi haiwezi kwenda kwa matakwa ya mtu binafsi kwa sababu njia ni moja na inatumiwa na magari ya kawaida na mabasi, hivyo hakuna muujiza wa kuyasogeza ili yawahi kuchukua abiria.
”Mbezi huwezi ukategemea mipango yako kwa sababu ile ni foleni na kuna wakati magari yanakata kabisa, hali ya barabara ndio inatafsiri aina ya huduma zitakayoendelea. Mbezi ni eneo ambalo barabara inatumiwa na magari mengine kwahiyo inategemea na mfumo wa barabara zingine zitakavyokuwa,” amesema Bugaywa.
Aidha, amesema kuwa mfumo utakavyokuwa kama kuna foleni lazima tu magari yatakwama kwenye foleni na hakuna muujiza wa kuyasogeza hapo na hata abiria wanajua na wamekuwa wakiwaelewesha katika hilo.
Hatua hiyo, imekuja mara baada ya kushuhudia hali ya foleni ya watu katika eneo hilo, walioonekana kukaa kwa muda mrefu bila gari kutokea.