Mbunge wa Jimbo la Vwawa kupitia CCM Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo, Japheti Hasunga amesema kuwa anakusudia kuwakutanisha vijana kwa ajili ya kongamano la kujadili fursa zilizopo katika sekta ya Kilimo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na vijana wa Jimbo la Vwawa katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi makao makuu ya Chama hicho Wilayani Mbozi.

Amesema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha na Kilimo, lakini miongoni mwao vijana ni wachache hivyo mkakati huo wa kuwakutanisha vijana ni sehemu ya kueleza fursa zilizopo kwenye sekta ya Kilimo na kuziendeleza.

Kuhusu kuimarisha masoko ya mazao mbalimbali ikiwemo zao la Kahawa, Hasunga amesema kuwa tayari wizara ya kilimo imeanzisha mkakati kabambe wa kuongeza minada ya kahawa ambapo kwa upande wa Kanda ya ziwa mnada utafanyika mkoani Kagera, Kanda ya Kaskazini utafanyika Manispaa ya Moshi, Kanda ya kusini utafanyika wilayani Mbinga na Kanda ya nyanda za juu kusini mnada wa kahawa utafanyika Wilayani Mbozi.

Aidha, amesema kuwa kuongeza minada ya uuzaji wa zao la kahawa utatoa fursa kwa wakulima kunufaika na mazao yao kwa kuuza kwa bei nzuri na kulipwa kwa wakati.

“Kumekuwa na mbegu nyingi mtaani ambazo sio sahihi kwa maana hiyo sasa serikali inachukua hatua kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo punde watakapobainika,” amesema Hasunga

Boko Haram wafanya shambulio mazishini, 65 wauawa vibaya
RC Mnyeti, Mbunge Ole Millya watibuana hadharani