Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amewaagiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za mitaa kupima, kulinda na kusimamia maeneo yote ya umma na maeneo ya wazi ili kuondokana na mwenendo mbaya unaoendelea kukithiri wa kuvamia maeneo hayo.

Dkt. Mabula ameyasema hayo hii leo Machi 29, 2023 Jijini Dodoma kwenye mkutano mkuu wa Nane wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji, na kukemea utaratibu mbaya na usiovumilika, wa kuvamia maeneo ya wazi, maeneo ya umma pamoja na yale hatarishi yanayobadilishwa kuwa ya matumizi mengine hasa makazi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula.

Amesema, maeneo hatari kimazingira pamoja na maeneo ya wazi, yakiwemo maeneo maalum kwa matumizi ya baadaye (land bank), yanapaswa kupimwa na kulindwa dhidi ya wavamizi na kwamba ili kuwa na miji nadhifu iliyopangwa vyema, hakuna budi kuanza kusimamia upangaji wa miji midogo na vitovu vya vijiji nchini.

“Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2022 inaonyesha kuwa miji inakuwa kwa asilimia 4.8 na taarifa tulizonazo tuna jumla ya miji midogo inayochipukia 4,310 Nchini ambayo isiposimamiwa ipasavyo itakuwa miji holela ya baadae,” amesema Dkt. Mabula.

Baadhi ya Wataalamu wa Mipango Miji wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Dkt. Angeline Mabula (hayupo pichani).

Aidha, ametoa maelekezo kwa Bodi ya Usajili Wataalam wa Mipango Miji na wanataaluma wote kuweka mkazo Zaidi katika namna ya kuzuia miji midogo na vijiji kuwa makazi holela ya baadae kwa kusimamia na kuelimisha jamii matumizi ya mwongozo wa upangaji na ujenzi wa nyumba bora vijijini.

Hata hivyo amesema gharama za kumudu kupanga, kupima na kumilikisha maeneo yote nchini ni kubwa, na hivyo kuelekeza Mamlaka za Upangaji nchini kutenga fedha kutokana na mapato ya ndani ya kila mwaka, kwa ajili ya kazi hiyo ya kupanga, kupima, kumilikisha, kuendeleza
na kusimamia miji katika maeneo yao.

Kuhusu suala la Mabadiliko ya tabia nchi, Waziri Mabula amesema ni muhimu kwa sasa katika sayansi ya usanifu wa miji duniani kote na kuongeza kwamba, “ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika miji yetu tunatarajia mchango mkubwa sana wa Wataalamu wa Mipango miji katika kuweka mifumo wezeshi kwa ajili ya kukabiliana na majanga mbalimbali kuanzia katika usanifu wa mipango.”

Mfahamu Kamala Harris, jembe lenye damu ya kihindi... anachoijia Tanzania
GGML, STAMICO wasaini mkataba wa bilioni 55.2 za uchorongaji