Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maelekezo katika Wiki ya nenda kwa usalama Barabarani ikiwemo kulitaka Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, kuhakikisha mchakato wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria na kanuni za usalama barabarani unafanyika kwa haraka, ili kuwa na sheria bora.

Maelekezo hayo, ameyatoa katika uzinduzi wa Wiki hiyo ya usalama barabarani Machi 15, 2023 na kuongeza kuwa, Baraza pia lifuatilie mfumo wa alama kwenye barabara na kwenye leseni za udereva, ili kuwabaini madereva wanaokiuka sheria na kuwachukulia hatua.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Amesema, pia Baraza linatakiwa kuharakisha utekelezaji kikamilifu maagizo ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa mwaka jana (2022), Mkoani Arusha kuhusu ukaguzi wa magari kwa kushirikisha wadau, ili lengo la ukaguzi lifanikiwe.

Aidha, Waziri Mkuu pia amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha kufunga mifumo ya kielektroniki itakayokuwa inabaini makosa mbalimbali, ili kusaidia na kufanya kazi kwa urahisi na kutoa taarifa ni nani anaendesha huku anatumia simu au kulewa na mwendokasi.

“Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, tuendelee na utaratibu wa sasa wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya watumia barabara. RTOs na timu zao, tuanze kuimarisha utaratibu wa kutoa elimu hii,” amesema Waziri Mkuu.

Kivuko cha waenda kwa miguu.

Aidha, amesema, “Wizara ya elimu ione haja ya kuanza kutoa elimu ya usalama barabarani kwa shule za msingi, sekondari na hata vyuoni ili vijana wasisikie leo tu, au kusubiri hadi raisi aseme na kamati za usalama barabarani za mikoa.”

“Kwa kushirikiana na TANROADS na TARURA, Wizara iyapitie upya maeneo ya barabara ambayo ni hatarishi, kuyaweka alama na kutoa elimu kwa watu wa maeneo hayo, pia tengenezeni utaratibu wa pamoja wa kushirikiana, ili kuepusha ajali za barabarani,” amefafanua Majaliwa.

Wanne wauawa kwa shambulio la bomu akiwemo Gavana
Nayib Armando Bukele: Rais Bishoo anayeacha alama Duniani