Kupitia taarifa yake iliyotangazwa moja kwa moja kwenye televisheni ya Taifa, Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern ametangaza kuwa atajiuzulu wadhifa wake ifikapo February 7, 2023.
Ardern amesema, hana mpango ya kuwania wadhifa huo kuchaguliwa tena katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 14, 2023 na kwamba anaamini chama chake cha Labour, kitashinda uchaguzi ujao.
Amesema, “sina nguvu na ari inayohitajika kwa kazi hii, kuiongoza nchi ndiyo kazi ya fahari ya juu zaidi mtu anaweza kuwa nayo, lakini ni kazi yenye changamoto nyingi, huwezi na hupaswi kuifanya kama huna nguvu na motisha ya akiba kukabili changamoto ambazo hazikutarajiwa.”
Ardern, alichaguliwa kuwa Waziri mkuu wa New Zealand mwaka 2017 alipokuwa na umri wa miaka 37, hivyo kuwa moja kati ya wanawake wenye umri mdogo ulimwenguni kuongoza serikali na ameshahudumu kwenye wadhifa huo, kwa miaka mitano na nusu.