Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Majaliwa amewataka Mabalozi hao wajifanyie tathmini kila mwisho wa mwaka mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika Mataifa ambayo ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Ametoa agizo hilo Aprili 8, 2018 wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Urusi, katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Majaliwa amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia katika kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri hivyo msisite kufanya hivyo huko muendako.”

Pia amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke nyumbani.

Amewasisitiza mabalozi hao kwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa Balozi kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia maslahi ya nchi lazima mkayasimamie huko muendako hasa katika masuala ya kiuchumi.”

Kwa upande wao mabalozi hao wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.

Omba omba, walemavu kutupwa jela
Video: Serikali yawarejesha kazini watumishi waliokuwa wamefukuzwa