Serikali imelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA), kwa kazi nzuri inayofanya na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya hifadhi na shirika hilo.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti Julai 23, 2022 na kupata maelezo ya utoaji wa habari kidijitali (Serengeti Media Center), katika kutangaza vivutio, shughuli za hifadhi na za jamii zinazozunguka hifadhi.
Akiwa eneo hilo, Dkt. Chana pia alikutana na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ambapo Mkuu wa Hifadhi hiyo Kamishna wa Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Izumbe Msindai alitoa taarifa fupi ya hifadhi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, William Mwakilema alimshukuru Waziri Chana kwa kutenga muda na kutembelea maeneo hayo ili kujionea shughuli mbalimbali za uhifadhi na utalii zinavyofanyika.
Kituo cha Serengeti Media Centre (SMC), kimeanza kufanya kazi na watalii wanapata taarifa mbalimbali za hifadhi na kitafunguliwa rasmi baada ya taratibu kukamilika.