Kikosi cha Young Africans kimewasili salama mjini jijini Lubumbashi nchini DR Congo, huku msafara wa kikosi hicho ukawajumuisha watu wazito sita ikiwa ni kuongeza nguvu kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya wenyeji, TP Mazembe.
Young Africans itavaana na TP Mazembe keshokutwa Jumapili (April 02) saa 10 jioni, ikiwa ndio mchezo pekee wa mchana kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho, huku mingine ikipangwa kupigwa usiku.
Licha ya kufuzu Robo Fainali, Young Africans ina kitu kizito inakisaka ikitaka rekodi ya kumaliza kama kinara wa kundi ili kukwepa kuangukia kwa timu vigogo zitakazomaliza nafasi ya kwanza na kutakiwa kuanzia michezo ya awali nyumbani na kumalizika ugenini.
Endapo Young Africans itamaliza wa kwanza itakutana na wepesi wa kukutana na timu zilizomaliza nafasi ya pili na faida kubwa katika Droo itakayofanyika juma lijalo, itawafanya waanzie ugenini na kumalizia nyumbani, kitu wanachokipigania kwa sasa wakiifuata Mazembe kwao.
Katika kuhakikisha mambo yanaenda sawa msafara wa Young Africans uliowasili jana Alhamis (Machi 30) majira jioni jijini Lubumbashi ukiwa na watu wazito wakiwemo wajumbe wawili wa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, Tarimba Abbas ambaye pia ni Mbunge wa Kinondoni na bosi wa SportPesa ambao ni wadhamini wakuu wa Young Africans, pia yumo Geofrey Mwambe ambaye ni Mbunge wa Masasi Mjini.
Mbali na hao yumo mfadhili wao aliyewarudishia jeuri ya ubora Ghalib Said Mohamed “GSM’ akiambatana na Mkuu wa Msafara wao, Lameck Nyambaya ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es salaam na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said na Makamu wake Arafat Haji.
Mara ya mwisho Young Africans kusafiri na msafara wa namna hii ilikuwa Julai 20 wakipotua Arusha kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na kulibeba taji kwa kuichapa Coastal Union kwa Penati.
Arafat amesema: “Tumefuzu, ila yapo malengo mengine ndio maana unaona tumesafiri na timu kamili na wale wengine ambao walikuwa timu za taifa tutakutana nao huko,” alisema Arafat ambaye mara ya mwisho kusafiri na Yanga akiwa na Hersi waliweka rekodi kuichapa Club Africain ya Tunisia na kufuzu makundi.”
Wakati kikosi cha Young Africans kikiondoka jana jijini Dar es Salaam, kocha wa timu hiyo Nasreddine Nabi hakuwa sehemu ya msafara huo kufuatia kuchelewa kurejea alipokwenda kwake Ubelgiji na kufanya mchakato wa kupata visa yake ya kuingia nchini DR Congo kuchelewa na anatarajiwa kuondoka leo Ijumaa (Machi 31).