Uongozi wa West Ham United unaamini Klabu za Manchester United Arsenal zitapigana vikumbo kwenye mpango wa kumsajili kiungo Declan Rice mwishoni mwa msimu huu.
West Ham wanaamini watapata mkwanja wanaotaka, Pauni 100 milioni na zaidi kwenye mauzo ya Kiungo huyo kutoka England, ambaye amekataa kusaini mkataba mpya.
Meneja wa miamba hiyo ya jijini London, David Moyes amekiri anatarajia kumpoteza nahodha wake huyo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Rice mwenye umri wa miaka 24, bado ana miaka miwili imebaki kwenye mkataba wake, lakini Uongozi wa West Ham Utd ulijipanga kumsainisha mkataba mpya, lakini mpango huo ulifeli.
Hivyo, wanadhani kupokea ofa ya Pauni 92 milioni na ziada kutoka Arsenal kiwango hicho hakitawatosha.
Ripoti zinafichua wamepanga kuweka bei ya juu wakiamini Man United nao watakuja na ofa ya juu zaidi ya Arsenal.
Sasa Arsenal imeriporiwa kuwaweka kwenye rada viungo wengine watatu kwa ajili ya kuwanasa wakimkosa Rice.
Meneja wa The Gunners Mikel Arteta bado anamtaka kiungo wa Brighton, Moises Caicedo baada ya ofa zake mbili kugomewa mwezi Januari mwaka huu.
Kiungo mwingine anayemtaka ni mkali wa Real Sociedad, Martin Zubimendi na jina la tatu ni la Ruben Neves wa Wolves, ambaye pia yupo kwenye rada za Man United na Liverpool.
Arsenal wanaamini Meneja wa Man United, Erik ten Hag ataweka mkazo kwenye usajili wa Mshambuliaji wa kiwango cha dunia, hivyo viungo watasubiri baadae kutokana na kuhusishwa na Harry Kane na Victor Osimhen ambao wote gharama yao ni kubwa.