Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imekutana na Makatibu Tawala wasaidizi sekta ya Viwanda,biashara na uwekezaji ngazi za Mikoa kwa ajili kuipitia rasimu ya mwongozo wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Akifungua warsha hiyo jijini Dodoma Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Conrad Milinga amesema nia ya serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara kuanzia ngazi za chini.
Milinga ameongeza kuwa, “tunataka mapato lazima tutengeneze watu ambao watatupa mapato suala la kuamka asubuhi unakwenda kufunga biashara ya mtu, tunataka tumjengee uwezo aone ana wajibu gani kwa serikali lisiwe suala la kusukumana, mtusaidie kutoa elimu ilia one Ofisa biashara ni msaada.”
Aidha, amesema wataalamu hao wataangalia mpango wa kuboresha mazingira ya biashara ikiwamo kuangalia ukuaji wa sekta binafsi na kuongeza kuwa Maofisa hao ni wasimamizi kwenye Mikoa na Halmashauri kuhusu sheria, sera, kanuni na taratibu.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara ,wizara ya uwekezaji na Biashara Sempeho Manongi amesema kuwa lengo la kuwaita watendaji hao ili kuwaelewesha na kuhamasisha ujengaji wa mazingira wezeshi ya kibiashara uwekezaji na Viwanda.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mororgoro, Beatrice Charles ,amesema kuwa muongozo huo unaenda kuwafanya kazi kwa uweledi na kwamba wataenda kuondoa vikwazo eneo la uwekezaji,na ujenzi wa viwanda itakayosaidia kuongeza mapato.