‘Wa Kimataifa’, Young Africans SC jana usiku ilionesha umahiri wa hali ya juu na kuibana mbavu timu ya Al Ahly katika mchezo ulioshuhudiwa Mjini Alexandria nchini Misri, licha ya kupoteza na kuondolewa kwenye michuano.

Yanga walionesha mchezo mzuri wakipambana na kasi ya Al Ahly pamoja na hujuma mbalimbali za mashabiki na wachezaji wa timu hiyo lakini walifungwa bao 2-1, hivyo kutolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya magoli 3-2 kwa kuwa mechi yao ya awali jijini Dar es Salaam ilimalizika kwa sare ya 1-1.

Al Ahly walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Yanga katika dakika ya 51, baada ya Hossam Ghaly kutumia vizuri fursa ya mpira wa kona.

Dakika 15 baadae, Yanga waliwanyamazisha Mashabiki wa Al Ahly baada ya Juma Abdul kumtoka beki wa Al Ahly na kupiga vizuri mpira uliotua kikwani kwa Donald Ngoma aliyezamisha kinywani. Hadi dakika 90 zinakamilika, ubao wa matokeo ulikuwa unaonesha 1-1.

Hata hivyo, Al Ahly walitunisha misuli zaidi katika dakika za nyongeza na kujipatia bao la pili katika dakika ya 95, baada ya mchezaji wake kuutumia vizuri mpira wa krosi iliyopigwa kutoka kulia na kuunganisha kwa kichwa.

Hata hivyo, mpira huo ulishuhudia vurugu za dakika kadhaa kati ya wachezaji wa timu hizo mbili, lakini pia katika kipindi cha kwanza mashabiki wa Al Ahly walijaribu kumhujumu Dida kwa kummulika na miale, lakini aliendelea kuwa imara.

Chadema - Mbeya wamsusia Mkuu wa Mkoa Amos Makalla, wadai amewapuuza
WAZIRI MKUU AONGOZA WAKAZI WA DODOMA MAZISHI YA ASKOFU ISUJA