Baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0, dhidi ya Mbeya City walioupata Jumapili iliyopita kikosi cha Young Africans, leo Jumamosi kinaivaa Tanzania Prisons kwenye wa Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Kikosi cha Young Africans kilicho chini ya Kocha kutoka nchini Zambia George Lwandamina, kitaingia kwenye mchezo huo kikionekana kuimarika zaidi kufuatia kurejea kwa baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi na Amissi Tambwe, ambao hawakuwepo kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Mbeya City.
Young Africans ambao ndiyo mabingwa watetezi wanaingia kwenye mchezo huo wakifahamu fika kuwa ushindi jambo pekee litakalo waweka kileleni japo kwa masaa na kuendelea kuwapa presha wapinzani wao Simba na Azam FC ambao wao mechi zao za mzunguko wa 11 wanacheza Jumapili na Jumatatu.
Mbali na kujivunia kuendelea kuimarika kwa kikosi chake lakini kocha Lwandamina bado ataendelea kuwategemea washambuliaji wake Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa aliyefunga mabao matatu kwenye ushindi wa mabao 5-0,dhidi ya Mbeya City.
Pamoja na kurejea kwa nyota hao lakini kikosi cha Young Africans hakitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa sana ingawa timu wanayocheza nayo siyo ya kubeza kutokana na uimara waliokuwa nao na ushindani waliouonyesha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba licha ya kupoteza mchezo katika dakika za mwishoni.
Patto Ngonyani na Rafael Daud walioonyesha kiwango cha juu dhidi ya Mbeya City wanatarajiwa kuanza kwenye eneo la kiungo wa juu na chini huku Emmanuel Martin naye akiendelea kutamba kwenye winga ya kushoto wakati Mcameroon Youth Rostand akikaa langoni kama ilivyo kawaida. katika mfumo ule wa 4-3-3.
Tanzania Prisons tayari wapo Dar es Salaam kwa siku kadhaa, na wamejipanga kuhakikisha wanawalipiza kisasi ndugu zao wa Mbeya City, ambao wiki iliyopita walikumbwa na aibu ya kipigo hicho,
Mshambuliaji tegemezi wa timu hiyo Mohamed Rashid, amesema ni mchezo mgumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapambana na kuwadhibiti Young Africans ili wasiweze kupata ushindi kwenye mchezo huo muhimu kwao.
Amesema wanajua Young Africans ni timu kubwa lakini uwezo wa wachezaji wao haupishani na ule wa wakwa hivyo wamedhamiria kupambana ili kupata angalau sare ili kuwavurugia mipango yao na wao kurudisha matumaini ya kufanya vizuri siku zijazo.
Wachezaji kama Lambart Sabyanka na Salum Kimenya wanatarajiwa kuanza kikosi cha kwanza kuipigania timu hiyo ambayo licha ya kufungwa na Simba lakini imeonekana bado ni imara na imekuwa ikipata matokeo mazuri inapocheza na wadogo wenzao.