Mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Young Africans MC Alger ya Algeria huenda ukafanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Imeripotiwa kuwa viongozi wa Young Africans wapo katika harakati za kufanikisha mpango wa kuuhamishia mchezo huo Mwanza kutoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa matarajio ya kupata watazamaji wengi na pato kubwa.

Tayari mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya wenyeji Mbao FC na Simba SC ya Dar es Salaam uliokuwa ufanyike Aprili 8, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba, umesogezwa mbele kwa siku mbili hadi Aprili, 10.

Lakini taarifa ya Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura leo imesema hatua hiyo imechukuliwa ili kupisha shughuli za kijamii kwenye Uwanja huo zitakazoanza Aprili 1 hadi 9.

Young Africans imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wauzaji na Wanywaji pombe aina ya viroba waja na mbinu mpya
Mashabiki Wa Kiafrika Wavamia Uwanja