Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi, amesema hawatarudia makosa kwenye mchezo ujao wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya US Monastir ya Tunisia.
Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo siku ya Jumapili (Machi 19) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikihitaji ushindi ambao utaivusha kwenda Robo Fainali ya Michuano hiyo.
Nabi amesema katika mchezo huo atahakikisha kikosi chake kinakuwa makini na kuhakikisha kinapata matokeo mapema, jambo ambalo litaongeza nguvu ya kujiamini na kucheza kwa utulivu.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema kuna ugumu kwenye michuano hiyo ya kutokana na kila timu kuhitaji ushindi hivyo, watajitahidi kupata matokeo mapema kuongeza nguvu ya kujiamini.
“Ikiwa tunakutana na timu imara ambayo inahitaji matokeo ni lazima tufanye kazi kubwa kwenye kutumia nafasi hasa zile za mwanzo zitatufanya tuwe imara na kupata matokeo mazuri.”
“US Monastir ni timu imara ina wachezaji wazuri hata wachezaji wetu nao ni wazuri hivyo makosa ambayo tulifanya kwenye mchezo uliopita tunayafanyia kazi,” amesema Nabi.
Young Africans iliyoshuka Dimbani mara nne katika michuano hiyo, ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi D ikiwa na alama 07, ikitanguliwa na US Monastir ya Tunisia yenye alama 10, huku TP Mazembe ya DR Congo ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 03 na AS Real Bamako ya Mali inaburuza mkia kwa kuwa na alama 02.