Uongozi wa Simba SC umetangaza rasmi kuanza kwa maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Soka wa Guinea Horoya AC.

Miamba hiyo itakutana Jumamosi (Machi 18) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Simba SC ikihitaji ushindi wa hali na mali ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Robo Fainali.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amezungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu (Machi 13) na kueleza kwa undani mipango ya maandalizi ya kuelekea mchezo huo ambao umepangwa kuchezwa kuanzia saa moja usiku.

Ahmed amesema, tayari kikosi chao kimeshaingia kambini kuanza maandalizi ya kuiakabili Horoya AC, tayari kwa mazoezi ambayo rasmi yanaanza leo Jumatatu.

“Mchezo wetu dhidi ya Horoya utakuwa ni Jumamosi hii na kikosi kimeingia kambini kujiandaa na mchezo huo. Jana Jumapili wachezaji walipumzika lakini leo tunaanza rasmi mazoezi.”

“Kibu Denis amepona na leo ataanza mazoezi na wenzake. Ni taarifa ya kufurahisha maana kila mmoja anajua ubora wa Kibu na namna alivyoimarika hivi karibuni.”

“Akili na nguvu zetu tunakwenda kuziweka Jumamosi ili tuweze kushinda na kufuzu Robo Fainali. Ni mechi yenye namna moja pekee tu kushinda. Mechi hii inatukumbusha mechi ya AS Vita, safari hii tupo na Horoya.”

“Kila Mwanasimba lazima atambue kwamba tutaingia Uwanja wa Mkapa kwenda kupambana kuingia Robo Fainali. Hatuko tayari kuishia hatua ya makundi na wakati mechi ya kutupeleka robo tutachezea Uwanja wa Mkapa.”

“Waamuzi wote wa mchezo wanatokea nchini Misri. Waamuzi hawa wanne watawasili nchini alfajiri ya Machi 17, 2023.”

Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa imejikusanyia alama 06 zinazoiweka kwenye nafasi ya Pili katika msimamo wa Kundi C, ikitanguliwa na Raja Casablanca ya Morocco iliyokusanya alama 12 baada ya kushinda michezo mine waliocheza hadi sasa.

Hoyora AC inashika nafasi ya tatu katika Kundi hilo ikiwa na alama 04 baada ya kucheza michezo minne, huku Vipers SC ya Uganda ikiburuza mkia kwa kuwa na alama moja.

Kispika cha Ahmed Ally kuanza Jumatano
Denis Nkane asubiri ruhusa ya Nabi