Kwa mara nyingine tena Uongozi wa Young Africans umemwandikia Barua Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ya kumtaka kurejea kambini kujiunga na wachezaji wenzake.
Young Africans imefanya hivyo, baada ya kukiri kupokea maamuzi ya marejeo ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu suala la kiungo huyo.
Taarifa ya Young Africans imeeleza kuwa, baada ya kupokea maamuzi hayo, Uongozi wa Klabu hiyo umemwandikia Barua Feisal Salum kumtaka aripoti kambini haraka iwezekanavyo na kuendelea kuutumikia mkataba wake kama mchezaji wao halali mpaka tarehe 30, Mei 2024, kama ilivyoamuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Hata hivyo taarifa hiyo imesisitiza Klabu ya Young Africans iko tayari kumpokea Feisal Salum na kumjumuisha kwenye kikosi, na kwa kuzingatia sera na utaratibu wa Klabu hiyo katika kuwaongezea mikataba wachezaji wake wanaofanya vizuri.
“Uongozi wa Yanga uko tayari kuendelea na mazungumzo na Feisal Salum Abdallah na wawakilishi wake juu ya kuboresha mkataba wake, kama wataridhia.” imeeleza taarifa hiyo
Katika hatua nyingine Young Africans imeuarifu umma kwamba, iko tayari kumruhusu Feisal Salum Abdallah kuondoka klabuni kwa kuzingatia matakwa ya mkataba na utaratibu wa sheria za uhamisho wa wachezaji zinazotambulika na TFF pamoja na FIFA.
Pia imetoa wito kwa klabu yoyote inayohitaji huduma ya mchezaji huyu, kufuata utaratibu ili kuanza mazungumzo wakati wowote.