Mshambuliaji kutoka Burkina Faso na klabu ya Ihefu FC Yacouba Sogne amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Februari wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2022/23, huku Mecky Maxime wa Kagera Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Yacouba amewashinda Medie Kagere wa Singida Big Stars na Elias Maguli wa Geita Gold alioingia nao Fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).

Kwa mwezi Februari, Yacouba alionesha kiwango kizuri ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kuhusika katika upatikanaji wa bao moja kwenye michezo miwili aliyocheza.

Ihefu FC kwa mwezi huo ilicheza michezo mitatu ikishinda miwili na kutoka sare mmoja na kupanda kutoka nafasi ya 11 hadi ya 8.

Kwa upande wa Maxime aliwashinda Nasreddine Nabi wa Young Africans na Fikirini Elias wa Coastal Union, ambapo kwa mwezi Februari, Kagera Sugar ilicheza michezo mitatu na kushinda miwili dhidi ya Namungo bao 1-0 na Ruvu Shooting bao 0-1, ikatoka suluhu na Polisi Tanzania hivyo kujikusanyia alama saba na kupanda kutoka nafasi ya saba hadi ya sita katika msimamo wa Ligi hiyo yenye timu 16.

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Highland Estates uliopo Mbarali mkoani Mbeya, Omari Malule kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Februari, kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Serikali yasitisha huduma za bweni darasa la awali-iv
Ahmed Ally: Vipers SC watajuta kuja Dar