Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umeweka wazi kuwa unahitaji kuvunja Rekodi ya Mabao waliyowafunga TP Mazembe kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Hatua ya Makundi.

Timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi Keshokutwa Jumatano (Machi 08) itakuwa na kibarua cha kusaka alama tatu dhidi ya AS Real Bamako, katika mchezo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Miamba hiyo ilikutana mwishoni mwa mwezi Februari mjini Bamako nchini Mali, na kuambulia sare ya 1-1, hivyo kila upande uliondoka na alama moja.

Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema kuwa wana kazi kubwa ya kufanya kwenye michezo ya kimataifa na kupata ushindi nyumbani ili kuongeza nguvu ya kufikia malengo ya kutinga Hatua ya Robo Fainali.

“Tulishinda mabao matatu dhidi ya TP Mazembe wakasema kwamba hatuwezi kufunga mabao mengi, sasa kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya AS Real Bamako tunahitaji kufunga mabao mengi zaidi.”

“Uzuri ni kwamba kuna wachezaji wazuri ambao wanafanya kazi kubwa, kila kitu tunaamini kwamba kitakuwa sawa na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu wa Jumatano.” amesema Kamwe

Hadi sasa Young Africans imeshakusanya alama 04 zinazoiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi D, ikitanguliwa na US Monastir ya Tunisia yenye alama 07, na TP Mazembe inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 03.

AS Real Bamako inaburuza mkia wa Kundi hiyo kwa kujikusanyia alama mbili zilizotokana na sare mbili mfululizo dhidi ya US Monastir na Young Africans, kabla ya kupoteza mbele ya TP Mazembe ya DR Congo.

Ahmed Ally: Vipers SC watajuta kuja Dar
Robertinho kutumia nyenzo za Juma Mgunda