Kukosekana kwa Watumishi wa afya katika Kijiji cha Bugogwa kilichopo kata ya Mwamala, kumesababisha Zahanati kufungwa na Wananchi kukosa huduma kwa zaidi ya miezi 11 sasa huku Serikali ikikiri tatizo hilo na kusema itapeleka Mtumishi haraka na huduma zianze.
Hayo yamebainishwa na Diwani Viti Maalum, Anna Pius wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu ya mwaka na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Nice Munisy kutoa maelezo kuhusu hali hiyo.
Amesema, “Wananchi sasa hivi wanapata huduma kwenye Zahanati ya Kijiji cha Mwamala na kituo cha Afya Samuye, maana Daktari aliyekuwepo alifariki na alibaki Muuguzi peke yake ambaye alidai hawezi kuwapa huduma wala kujaza madokezo.”
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri, Nice Munisy alisema hana taarifa za kufungwa kwa zahanati hiyo, ambapo Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Nuru Yahya akikiri kufungwa kwa Zahanati na kuomba radhi, huku akiahidi kumpeleka mtumishi haraka ili Wananchi waanze kupata huduma.