Zaidi ya watu 400 wameuawa na wengine zaidi ya 3,500 kujeruhiwa katika mapigano yanayoendelea nchini Sudan, baina ya vikosi vya jeshi rasmi na jeshi la dharura.
Msemaji wa Shirika la Afya Duniani – WHO, Margaret Harris ameyasema hayo mjini Geneva na kuongeza kuwa vituo 20 vya afya vimesimama kazi na vingine 12 viko katika hatari ya kuacha kutoa huduma.
Amesema, hali hiyo sio tu inaathiri watu waliojeruhiwa wakati wa mapigano, bali pia wale waliokuwa wakihitaji matibabu hapo kabla huku Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa – UNICEF, likisema watoto tisa ni miongoni mwa waliouawa na 50 wamejeruhiwa.
Taarifa ya msemaji wa UNICEF, James Elder, imeeleza kuwa mapigano ya Sudan yamechangia familia nyingi kukwama majumbani zikiwa hazina umeme, chakula, maji na madawa.