Ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka 2014/2015,umebaini kuwa kiasi cha shilingi milioni 951 kimelipwa kwa kazi ‘hewa’ kwa kazi za Kandarasi katika taasisi 9 za serikali.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya PPRA jijini Dar es Salaam.

Balozi Matern Lumbanga alifafanua kuwa kiasi hicho kililipwa kwa kazi ambazo hazikufanyika na kwamba kimekadiliwa kuwa sawa na asilimia 15 ya jumla ya thamani ya miradi yote ya kazi za ujenzi zilizokaguliwa na Mamlaka hiyo.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Halmashauri ya Kigoma (Shilingi milioni 11.1), Halmashauri ya Kibondo (Shilingi milioni 64.9), Halmashauri ya Jiji la Mwanza (Shilingi Milioni 69.6), Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Shilingi milioni 25.42), TANAPA (Shilingi milioni 156.3), Mamlaka ya Reli Tanzania (Shilingi milioni 473.6), Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe (Shilingi milioni 93.09) na Halmashauri ya wilaya ya Kwela (Shilingi Milioni 2.08).

Aidha Balozi Lumbanga alieleza hatua ambazo Mamlaka hiyo itachukua dhidi ya taasisi hizo, “Kwa upande wa malipo kwa wakandarasi kwa kazi ambazo hazikufanywa, PPRA itapeleka timu ya wataalam kuhakiki malipo hayo. Timu hiyo itahusisha wakandarasi na wataalam washauri waliohusika na miradi hiyo, meneja wa miradi na taasisi nunuzi husika.”

 

Hawa Ni 10 Bora Kwa Mujibu Wa Sokkaa.com
Zawadi Ya Khanga Ya 'Kijani' Yazua Tafrani kwenye ‘Kitchen Party’