Wakata miwa kutoka Manungu, Tuariani mkoani Morogoro Mtibwa Sugar wameanza tambo za kufanya vyema msimu huu wa 2017/18, kufuatia kikosi chao kushinda michezo miwili ya ligi hiyo na kuwafanya kuwa kileleni mwa msimamo.

Kocha Zuber Katwila, amekua wa kwanza kuwasilisha tambo zake katika vyombo vya habari kwa kusema msimu huu, amejipanga kurejesha heshima ya klabu hiyo iliyopotea zaidi ya muongo mmoja kwa kushindwa kutwaa ubingwa, huku akikanusha timu yake imebahatisha.

Timu ya Mtibwa Sugar imepania kuonyesha maajabu msimu huu kwa kuendeleza kasi iliyoanza nayo na kutwaa ubingwa au kumaliza ligi kwenye nafasi mbili za juu.

Hayo yamesemwa na kocha Zuber Katwila, aliyeiongoza timu hiyo kushinda michezo miwili na kuziacha Simba, Yanga na Azam ambazo zimejikusanyia pointi nne katika idadi kama hiyo ya mechi walizocheza.

Katwila amesema msimu huu wamepania kufuta tuhuma zinazowakabili za kufanya biashara baada ya kujikusanyia pointi ambazo zinawapa uhakika wa kutoshuka daraja.

“Watu wengi wanaponda kasi yetu ambayo tumeanza nayo wengi wanasema tunaanza kwa kasi lakini mzunguko wa pili baada ya kupata uhakika wa kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao tunauza mechi jambo ambalo siyo kweli lakini tumejipanga kulithibitisha hilo kwa kuhakikisha tunatwaa ubingwa au kumaliza ligi kwenye nafasi mbili za juu,”alisema Katwila.

Kocha huyo ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa kabla ya kustaafu na kuhamia kwenye ukocha alisema , tuhuma hizo zinachafua jina lao na kitu ambacho amepania kuwaanda vyema wachezaji wake ili waweze kupambana hadi mwisho wa ligi ili kuthibitisha hilo.

Amesema Mtibwa ni timu kubwa na Kongwe kama ilivyo kwa baadhi ya timu na ndiyo maana waliwahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, mwaka 1999 na 2000,  hivyo tuhuma hizo hazina ukweli kwao kutokana na historia waliyokuwa nayo kwenye ligi.

Misimu kadhaa iliyopita hivi karibuni Mtibwa Sugar imekua na rekodi ya kufanya vizuri kwenye mzunguko wa kwanza, lakini pindi inapoanza mzunguko wa pili mambo huwa tofauti kwani huanza kupoteza mechi mara kwa mara na mara nyingi ushindi wake huwa ni sare.

Chadema yaomba msaada Ujerumani, EU matibabu ya Lissu
Video: Rick Ross aachia 'Santorini Greece'