Chama cha soka nchini Sweden kimetangaza mshambuliaji wa Man Utd Zlatan Ibrahimovic kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa nchi hiyo kwa mara ya 11 mfululizo.

Zlatan ambaye tayari ameshastaafu kuitumikia timu ya taifa lake, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo, kufuatia mambo makubwa anayoendelea kuyafanya katika uwanja wa soka kwa sasa.

Sifa za kumuwezesha kushinda tuzo ya mwaka 2016, zimetokana na uwezo na umahiri wake aliouonyesha akiwa na timu ya taifa katika fainali za barani ulaya (Euro 2016), klabu ya PSG ambayo ndio bingwa wa soka nchini Ufaransa pamoja na Man Utd.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36, alitangaza kustaafu soka huku akiacha kumbu kumbu ya kucheza michezo 114 na kufunga mabao 62, likiwepo bao la ajabu dhidi ya England ambalo alifunga kwa Ticktack akiwa katika umbali mrefu dhidi ya lango la The Three Lions mwaka 2012.

Hatua ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora kwa mara ya 11 inamuweka Ibra katika historia ya kipekee nchini Sweden, kwani haijawahi kutokea mchezaji kushinda tuzo hiyo mara nyingi zaidi tangu utaratibu huo ulipoanzishwa mwaka 1946.

Ridhiwani aeleza kwanini hufanya ibada ya Mizimu
Lissu Pasua Kichwa, Hakimu amuuliza Wakili wa Serikali ‘Mnamuogopa?’