Kiungo wa majogoo wa jiji Liverpool Adam Lallana amekubali kusiani mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Anfield.

Lallana amefikia makubaliano na uongozi wa Liverpool na kusaini mkataba utakaomuwezesha kukaa klabuni hapo hadi mwaka 2020.

Lallana, mwenye umri wa miaka 28, alijiunga na Liverpool akitokea Southampton Julai 25 – 2014, kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 25, na mpaka sasa ameshacheza michezo 80 na kufunga mabao 16 akiwa na wekundu hao wa Anfield.

Mkataba mpya wa miaka mitatu, utamuwezesha kiungo huyo kutoka nchini England kulipwa mshahara wa Pauni 110,000 kwa juma.

“Ninajihisi furaha baada ya kukamilisha jambo hili la kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hii, ninaamini uwezo na uwajibikaji wangu ndio siri ya mafanikio ya kuhitimisha suala hili muhimu,” Lallana aliiambia tovuti ya Liverpool.

“Hapa ni mahala sahihi kwangu, maana tangu nimekuja nimekua ninacheza kwa uhuru na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa kila mmoja anaehusika na timu, wakati nikiwa kwenye mchakato wa kusaini mkataba mpya, karibu wachezaji wote walinisisitiza nikubalia kufanya hivyo kutokana na kuhitaji mchango wangu ili kufikia lengo la kuipeleka mbele Liverpool.”

Lallana anakuwa ni muendelezo wa kampeni ya uongozi wa klabu ya Liverpool ya kuwasainisha mikataba mipya wachezaji klabuni hapo, mwezi uliopita walimalizana na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Philippe Coutinho, aliyesaini mkataba wa miaka mitano.

Video: Rais wa Uganda, Shelisheli kutembelea Tanzania
Brown Ideye Aongeza Idadi Ya Waafrika China